Notice: A session had already been started - ignoring session_start() in /home/tafirig/public_html/common.php on line 2

Warning: Cannot modify header information - headers already sent by (output started at /home/tafirig/public_html/makala.php:59) in /home/tafirig/public_html/common.php on line 3

MAKALA

MRADI WA KUJENGA UBIA KATI YA SEKTA BINAFSI NA SERIKALI KATIKA KUONGEZA UZALISHAJI KWENYE UFUGAJI WA SAMAKI

20/10/2017

Utangulizi
Sekta ya uvuvi huchangia kwenye uchumi wa nchi, usalama wa chakula na hali ya maisha au kwenye kipato cha watu. Lakini kutokana na ongezeko la watu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, mahitaji ya samaki yameendelea kuongezeka siku hadi siku, hivyo kusababisha uzalishaji samaki kutoka kwenye vyanzo vya asili kupungua kwa kasi sana. Ufugaji samaki hutoa fursa mbadala na endelevu, hivyo kupunguza pengo kubwa lililopo la upatikanaji na mahitaji ya samaki. Hivyo, kuna haja kubwa ya kuwekeza kwenye utafiti na uzalishaji katika tasnia ya ufugaji samaki.

Andiko la Mradi
Kwa kutambua fursa na changamoto katika tasnia hii, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kwa kushirikiana na taasisi za Utafifi wa Uvuvi Uganda (NaFFIRI) na Kenya (KMFRI) zilibuni Mradi wa kikanda wa ufugaji samaki kupitia Taasisi ya kuboresha Utafiti wa Kilimo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (ASARECA) kupitia programu za Mifugo na Uvuvi. Mradi huu ulilenga kuongeza tija, ongezeko la thamani na ushindani wa ufugaji wa samaki katika ukanda huu ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa kuanzisha ubia kati ya watafiti na wadau wote walioko katika mnyororo wa thamani wa ufugaji samaki kama vile: wazalishaji wa vifaranga vya samaki, wafugaji wa samaki, wasambazaji wa vyakula vya samaki na wafanya biashara wa samaki. Hivyo,Mradi huu ukafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia ASARECA, ambapo Tanzania tulipata jumla ya Dola za Kimarekani 238,946 sawa na takribani Shilingi za Kitanzania 370,366,300/= kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari, 2012 hadi Desemba, 2013.

Lengo la Mradi
Lengo la Mradi lilikuwa ni kuchangia maendeleo endelevu na ongezeko la ukuaji wa sekta ya ufugaji samaki na soko lake katika ukanda wa nchi za Mashariki na Kati mwa Afrika; na kuongeza tija, na pia ongezeko la thamani na soko. Aidha mradi ulilenga kuongeza uvumbuzi katika ufugaji wa samaki ili kuboresha hali ya maisha na kipato kwa wadau wote walio katika mnyororo tajwa hapo juu.

Utekelezaji wa Mradi
1.Kuchunguza hali halisi ya ufugaji wa samaki katika Kanda ya Ziwa Viktoria Uchunguzi wa awali uliofanyika Kanda ya Ziwa Viktoria katika mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza kabla ya ujio wa Mradi ulionyesha kuwa, hali ya ufugaji samaki katika Kanda ya Ziwa siyo nzuri sana. Iligundulika kuwa ukosefu wa mbegu (vifaranga) na vyakula bora vya samaki, pia elimu duni juu ya ufugaji wa samaki ni baadhi ya changamoto zinazowakabili wafugaji katika Kanda ya Ziwa. Sato aitwaye kwa kitaalam Oreochromis niloticus na Kambale mumi aitwaye Clarias gariepinus ndiyo samaki wafugwao kwa wingi katika eneo hili. Hii ni kutokana na uvumilivu wa samaki hawa katika mazingira ya kwenye mabwawa na urahisi wa upatikanaji wa chakula kinachofaa katika ufugaji wake.

2.Kuzalisha mbegu bora za samaki
TAFIRI kupitia Mradi huu wa ASARECA ilikarabati nyumba ya kuzalishia samaki aina ya Kambale mumi na kujenga mabwawa kwa lengo la kuzalishia vifaranga bora vya samaki aina ya Sato na kufanya tafiti mbalimbali katika ufugaji. Kwa vile Kambale mumi hawatagi kiasili katika mabwawa, Taasisi iliwazalisha kwa kutumia teknolojia mbadala ili kuhakikisha kuwa vifaranga vinapatikana. Vifaranga vya Sato na Kambale hivi sasa vinasambazwa kwa wafugaji wa samaki kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Kanda ya Ziwa.

3.Kutengeneza vyakula bora vya samaki
Kwa vile changamoto ya vyakula vya samaki imekuwa ni kubwa kwa wafugaji wengi wa samaki ikisababisha kutopata uzalishaji uletao tija, Taasisi ilifanya utafiti na kutengeneza vyakula bora vya samaki. Taasisi ilitengeneza vyakula vya aina mbili vinavyojulikana kama TAFIRI I na TAFIRI II kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yetu. Kati ya aina hizo mbili, chakula aina ya TAFIRI I kimeonekana kufanya vizuri zaidi ya kile kingine na hivyo kupendekezwa kuzalishwa kwa wingi na kusambazwa kwa wafugaji wa samaki. Pia kuhamasisha wananchi kuwekeza katika kuzalisha vyakula vya samaki ili kuiendeleza tasnia hii ya ufugaji wa samaki.

4.Kujenga uwezo wa wafugaji na watafiti katika ufugaji samaki
Wafugaji wengi wamekuwa wakipata mavuno kidogo kwa sababu ya kukosa usimamizi mzuri wa mabwawa yao, hasa kuanzia kwenye uandaaji na utunzaji wa mabwawa na pia kwenye ulishaji wa samaki katika mabwawa. Wananchi kwa kushirikiana na watafiti wameelekezwa namna ya kuandaa mabwawa, kulisha na kutunza samaki katika mabwawa ya kuchimbwa ardhini, matanki na katika vizimba. ​

5.Kujenga uelewa wa bidhaa za ufugaji wa samaki
TAFIRI kupitia kitengo cha Sayansi ya Jamii cha Taasisi, ilifanya utafiti wa kuangalia namna samaki wanaofugwa wanavyokubalika kwenye soko. Baadhi ya walaji, hasa kutoka katika maeneo ambayo teknolojia ya ufugaji bado iko chini, wamekuwa na hisia kuwa samaki hao hawana ubora kutokana na kuwa na harufu ya tope. Lakini baada ya kuwaongezea thamani samaki hawa kwa kuwachakata na kutengeneza bidhaa kama vile sambusa na kababu za samaki, kuwakaanga na kuwakausha kwa moshi, walaji wengi walikimbilia zaidi bidhaa hizi kuliko zile za samaki wanaoishi kwenye maji ya asili. Hata walaji ambao walikuwa hawampendi Kambale mumi, walibadilisha mtazamo huo baada ya kuonja bidhaa zilizotengezwa kutokana na samaki huyu. Kwa ujumla bidhaa zilizotengenezwa na samaki huyu zilipendwa zaidi.

SAIX 02/09/2017 17:52:26 PM
this z great Reply
MANJALE MASELE 25/02/2019 09:06:57 AM
Naomba kupewa ushauri katika eneo la ufugaji wa sato na kambale Reply
BUTTA, SHIJA NCHUNGWA 14/04/2020 13:48:59 PM
Tafiti inauhalisia wa hali halisiReply

Leave your comment here

Your comment will be posted after it is approved.
Name(required)* E-mail(optional)
Comments(required)*
Notify me of new comments to this post by email

Warning: include_once(language.php): failed to open stream: No such file or directory in /home/tafirig/public_html/footer.php on line 2

Warning: include_once(): Failed opening 'language.php' for inclusion (include_path='.:/opt/cpanel/ea-php56/root/usr/share/pear') in /home/tafirig/public_html/footer.php on line 2