DKT. BITEKO ASHUHUDIA MATUMIZI YA TAFITI BUNIFU ZA TAFIRI KATIKA MKUTANO WA UVUVI MDOGO AFRIKA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Mashaka Biteko (MB) (Wa kwanza mbele kulia) amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (Mgeni rasimi) katika Mkutano wa Uvuvi Mdogo Afrika 2024 uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Juni 2024. Mhe. Dkt. Biteko alitembelea Banda la Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ambapo alipokelewa na Mkurugenzi wa Utafiti, Maendeleo na Uratibu Dkt. Merry Kishe (Wa kwanza Kushoto). Dkt. Kishe alielezea majukumu makuu ya TAFIRI, ikiwemo kufanya utafiti, kuhamasisha, pamoja na kuratibu shughuli mbalimbali za uvuvi.

Dkt. Kishe aliendelea kuelezea kuwa TAFIRI imefanikiwa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi kwa kutumia tafiti bunifu. Moja ya tafiti hizo ni matumizi ya mfumo wa PFZ ‘Potential Fishing Zone’ unaolenga kusaidia wavuvi wadogo wa ukanda wa Bahari ya Hindi kutambua maeneo yenye viashiria vya samaki, pamoja na kutoa taarifa za masoko ya kuuzia samaki kupitia mfumo wa kidigitali wa "VUA na UZA Kidigitali". Mfumo huu unawawezesha wadau kutunza kumbukumbu za shughuli nzima ya uvuvi.

Mhandisi Innocent Sailale (Wa tatu kutoka kushoto) kutoka TAFIRI-Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) alionesha mbele ya mgeni rasmi jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi, akitumia simu kuonyesha utendaji wake.

Mkutano huu wa Uvuvi Mdogo Afrika 2024 umeleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi ili kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuendeleza uvuvi mdogo barani Afrika.

Post a comment