WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGUA RASIMI MKUTANO WA 8 WA OACPS JIJINI DAR ES SALAAM

Dar es Salaam, 11 Septemba 2024 - Mhe. Kassim M. Kassim (Wa tatu kutoka kushoto), Waziri Mkuu wa Tanzania na Mgeni Rasmi, ameongoza hafla ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa 8 wa Ushirika wa Nchi za Afrika, Karibiani, na Pasifiki (OACPS) uliondaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Tanzania), ulioanza leo jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo unalenga kupanua juhudi za kukuza bahari endelevu na zenye ustahimilivu, pamoja na kusimamia maji ya ndani, uvuvi, na ufugaji wa samaki katika nchi za OACPS. Mkutano huu unajikita katika masuala muhimu ya mazingira na maendeleo endelevu ya rasilimali za bahari na uvuvi.

Baada ya ufunguzi rasmi, Waziri Mkuu Mhe. Kassim M. Kassim aliwaongoza wageni waalikwa kutembelea mabanda mbalimbali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, likiwemo banda la Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), pamoja na mabanda ya wadau wengine yaliyotayarishwa kwa ajili ya kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa kupitia sekta ya uvuvi.

Mkutano huu umeanza rasmi katika ukumbi wa Mwl. Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo wadau mbalimbali kutoka mataifa wanachama wa OACPS wanashiriki katika kujadili na kutafuta mbinu za kudumisha maendeleo katika sekta ya bahari na uvuvi.

Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika, Karibiani, na Pasifiki katika kulinda na kutumia kwa ufanisi rasilimali za bahari na maji ya ndani kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Post a comment