WAVUVI WABAINI MNYAMA BAHARI (POMBOO) AKIELEA KATIKA UFUKWE WA DAR ES SALAAM

Leo Tarehe 30 September 2024: - Wavuvi wa Mbweni Jijini Dar es salaam Waliona Mnyama Bahari (Pomboo) wa ukubwa usio wa kawaida akielea ufukweni. Tukio hilo liliwakusanya wavuvi pamoja na wakaazi wa eneo la Mbweni Pwani kwenda kushuhudia.

Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wavuvi Bw, Gilbert Paschal, ambaye ni Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Manispaa ya Kinondoni anayesimamia ukanda wa Mbweni, alitoa taarifa kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kituo cha Dar es salaam ili kufika kuchunguza kifo cha Mnyama Bahari huyo.

Timu ya watafiti kutoka TAFIRI ikiongozwa na Dkt. Catherine Mwakosya (Wa nne kutoka kushoto), ilifika katika eneo la tukio na kuweza kumtambua mnyama huyo aina ya Pomboo. Uchunguzi wa awali uliofanywa na Watafiti ulibaini uwepo wa majeraha mawili makubwa katika sehemu ya kati ya mwili ubavuni upande wa kulia, iliyoashiria huenda aligongwa na kitu chenye ncha butu. Maeneo mengine ikiwemo kichwa na sehemu ya mkiani hayakuwa na majeraha. Alikuwa Pomboo jike mwenye urefu wa mita 4.02, na kilo 650. Zoezi la upasuaji lilifanyika na kubaini viungo vyote vya ndani havikuwa na dosari yoyote. Sampuli ya mnofu, kipande kidogo kutoka pezi la ubavuni upande wa kushoto na kipande kingine kutoka pezi la mkiani vilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi kupitia DNA. Lengo kuu hasa ni kuthibitisha utambuzi wa awali na kutoa taarifa ya upatikanaji wake katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.

TAFIRI inawapongeza na kuwashukuru Jamii ya Wavuvi wa Mbweni kwa kuwa na uelewa na kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwepo kwa viumbe tofauti na vile walivyovizoea katika maeneo yao ya uvuvi.

Post a comment