TAFIRI NA IHE DELFT WAENDESHA WARSHA YA UCHAMBUZI WA TAKWIMU ZA EKOLOJIA BONDE LA MTO MARA

Tarehe 16-17 Oktoba 2024, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kituo cha Mwanza, kwa kushirikiana na IHE Delft kutoka Uholanzi, kinaratibu warsha ya siku mbili yenye lengo la kuboresha uwezo wa watafiti katika uchambuzi wa takwimu za ekolojia. Warsha hii ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utafiti wa mazingira, hususani katika maeneo yenye umuhimu wa ekolojia kama vile bonde la Mto Mara. Wawakilishi wa IHE Delft, Dkt. John Simaika na Prof. Ken Irvine, walitoa mafunzo ya kitaalamu kwa washiriki. Kwa upande wa TAFIRI, Dkt. Benedicto Kashindye, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TAFIRI-Mwanza, na Bi. Tausi Khitentya, Afisa anayeongoza Kituo Kidogo cha TAFIRI-Sota, walielezea umuhimu wa takwimu za ekolojia katika kufanya maamuzi kwa misingi ya kisayansi na sera. Warsha hii pia imehudhuliwa na watafiti waandamizi kutoka TAFIRI Mwanza, na Kituo Kidogo cha Sota, ambao wameonyesha ari kubwa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu. Kupitia warsha hii, washiriki wamepata fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi, na pia kuangalia takwimu zilizokusanywa na TAFIRI na IHE Delft. Takwimu hizi zinahusu tafiti za eekolojia zinazofanyika katika eneo la Bonde la Mto Mara, kwa msaada wa mpango wa Darwin Initiative. Lengo ni kuboresha uelewa wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za maji na samaki. Warsha hii ni sehemu muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za ndani na nje, na inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya utafiti wa mazingira nchini Tanzania. Aidha, warsha hii inatarajiwa kuchangia katika kuimarisha tafiti za eekolojia, sanjari na kuboresha uhusiano wa kitaaluma kati ya TAFIRI na IHE Delft, na kuimarisha uwezo wa watafiti wa TAFIRI katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na mazingira. Hii ni fursa muhimu kwa washiriki, na inatarajiwa kuleta matokeo bora katika utafiti wa mazingira na usimamizi wa rasilimali za maji.

Post a comment