Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imeshiriki warsha ya siku tatu iliyofanyika mkoani Mara kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba 2024. Warsha hiyo, iliyoandaliwa chini ya mradi wa "Usimamizi wa Uvuvi wa Jamii katika Bonde la Mto Mara.
Lengo kuu la warsha lilikuwa kupitia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, na kujadili namna bora ya kufikia malengo yaliyosalia kwa miezi sita ya mwisho ya mradi huo.
Washiriki walijadili fursa mpya za kutafuta fedha kwa kuandika miradi mingine ili kuhakikisha uendelevu wa Bonde la Mto Mara na mazingira ya bonde hilo yanabaki salama kwa vizazi vijavyo. Warsha hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano wa washirika mbalimbali wa kimataifa na kitaifa walioko mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira, wakiwemo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Shirika la WWF, Taasisi ya Elimu ya Maji (IHE Delft), Taasisi binafsi(Victoria Farming and Fishing Organization, VIFAFIO), Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mara, , Vikundi vya Ulindi wa rasilimali za uvuvi (Community management Unit (CMU), na Beach management Unit, Ofisi za halmashauri za wilaya zinazopakana na bonde la Mto Mara na Ofisi za Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB).
Washirika hawa wana jukumu muhimu katika kuhakikisha kuwa maliasili na uvuvi katika Bonde la Mto Mara zinatunzwa na kusimamiwa ipasavyo kwa manufaa ya jamii na mfumo wa ekolojia.
TAFIRI, iliwakilishwa na Dkt. Benedicto B. Kashindye, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo (Wa pili kutoka kushoto), pamoja na watafiti waandamizi, Bw. Joseph O. Luomba (Wa pili kutoka kulia, nyuma) na Bi. Magreth Musiba (Wa tatu kutoka kushoto). Uwepo wao ulidhihirisha dhamira ya TAFIRI ya kuendelea kuchangia katika juhudi za kitaifa na kimataifa za uhifadhi wa rasilimali za uvuvi na mazingira, hususani katika maeneo nyeti kama Bonde la Mto Mara.
Warsha hii imeonyesha umuhimu wa ushirikiano wa washirika katika kulinda na kuhifadhi rasilimali hizi adimu. Matokeo na mapendekezo yatokanayo na warsha hii yanatarajiwa kuwa dira ya kuhakikisha uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara na kuhakikisha kuwa jamii zinazoishi kandokando ya bonde hili zinanufaika kwa muda mrefu. .
Post a comment