TAFIRI Kituo cha Mwanza, kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Mfawidhi ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Mkoa wa Mara, imeendesha warsha ya kuwajengea uwezo wakufunzi ambao wataenda kutoa elimu kwa wadau wa uvuvi kuhusu ufuatiliaji, udhibiti na uangalizi wa rasilimali za uvuvi katika Bonde la Mto Mara. Mafunzo hayo yalihudhuriwa na maafisa uvuvi kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na halmashauri za Serengeti, Rorya, Butiama, na Tarime.
Washiriki wengine katika warsha hiyo walikuwa ni kamati za doria za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi vya Rasilimali za Uvuvi (BMU/CMU) kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Magatini (Serengeti), Nyabange na Kirumi (Butiama), Kinesi na Kwibuse (Rorya), na Kembwi (Tarime). Warsha hiyo iliongozwa na Mtafiti Mwandamizi ndugu Fenant L. Mhagama (Mtafiti) (Wa tatu kutoka kulia) , Bi. Kalwa O. Khamis (Mtafiti)(Wa pili kutoka kulia) na Afisa Mfawidhi wa Ofisi ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Mkoa wa Mara ndugu Yohana Mirumbe. Mada zilizowasilishwa katika warsha hii zilihusu kanuni muhimu za uvuvi, ambazo zilijumuisha marufuku ya matumizi ya zana haramu katika Ziwa Victoria na Mto Mara, pamoja na maelezo ya adhabu kwa makosa mbalimbali ya kukiuka kanuni za uvuvi na faini zake. Vilevile, washiriki walijengewa uwezo wa namna ya kufanya doria kwa ufanisi na ujazaji wa fomu zinazohusiana na kukiri makosa, ulipaji wa faini, na taratibu zinazotumika wakati wa kushikilia zana haramu za watuhumiwa. Pia walielimishwa kuhusu hatua za upokonyaji wa zana haramu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Afisa mwenye mamlaka ya kukamata. Baada ya mafunzo washiriki walikabidhiwa nakala za mada za mafunzo pamoja na mabango yenye mada muhimu ambazo zitatumika wakati wa kwenda kuwajengea uwezo wadau wa uvuvi katika vijiji wanavyotoka. Mradi huu wa usimamizi shirikishi wa ardhioevu ya Mto Mara umefadhiliwa na Darwin Initiative ya Uingereza na unatekelezwa na TAFIRI kwa ushirikiano na WWF Tanzania, Halmashauri za Wilaya zinazopakana na Bonde la Mto Mara na Ofisi za Bonde la Ziwa Victoria. Mafunzo haya yanatarajiwa kuboresha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi, kuhakikisha ulinzi na utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa lishe bora na kuboresha kipato kwa jamii zinazopakana na bonde la Mto Mara.
Post a comment