Dar es Salaam, Tanzania — Katika juhudi za kukuza na kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kuboresha maisha ya wavuvi wadogo, wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (International Fund for Agricultural Development IFAD), pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wametembelea Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Makao Makuu, kuangalia maendeleo ya Mradi wa Vikusanya Samaki (Fish Aggregating Devices - FADs). Mradi huu ni kati ya miradi inayofadhiliwa na IFAD kupitia Mpango wa Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi (Agriculture and Fisheries Development Programme, AFDP-2027), Tanzania inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza uzalishaji wa samaki na kuboresha ustawi wa wavuvi wa pwani ya Tanzania.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulipokelewana Mkurugenzi wa Uendelezaji tafiti na Uratibu wa TAFIRI, Dkt. Mary A. Kishe (Wa pili kutoka kulia). Dkt. Kishe alitoa maelezo ya kina kuhusu hazina ya maji iliyopo Tanzania na jinsi TAFIRI inavyotekeleza miradi ya Utafiti katika kuhakikisha pamoja na mambo mengine kwamba malengo ya Wizara ya Uvuvi endelevu na kuongeza uzalishaji wa samaki na rasilimali zingine za Uvuvi yanatimia. Aidha, Dkt Kishe alieleza maendeleo ya mradi huo tangu kuzinduliwa kwake, akieleza lengo la mradi, utekelezaji na mafanikio yake tangu uzinduzi rasmi wa mradi huu. “Tupo kwenye hatua nzuri sana za utekelezaji wa mradi huu ambao ni wa muhimu sana na tunatarajia kuwa utaleta matokeo chanya na ahueni kubwa kwa wavuvi na kwa uchumi wa Taifa kwa ujumla wake,” alisema Dkt. Kishe. Dkt. Happy K. Peter (Wa tatu kutoka kulia) ambaye ni msimamizi, wa Mradi wa FAD upande wa TAFIRI, alifafanua jinsi vifaa hivyo unavyofanya kazi na jinsi vitakavyonufaisha wavuvi wadogo wadogo. Alieleza kuwa teknolojia ya FAD husaidia kuvutia makundi ya samaki na kwa vile lengo ni kuwapunguzia gharama za uvuvi, mradi utaweka FADs karibu na maeneo wavuvi wanayovua, hivyo kupunguza muda na gharama za uvuvi. “Mradi huu unalenga kuhakikisha wavuvi wanavua kwa tija zaidi kwa kutumia mbinu za kisasa zinazopunguza muda na gharama za uvuvi,” alisema Dkt. Happy. Ujumbe kutoka IFAD na maafisa wa Serikali walionyesha kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza miradi kama hii inayochangia kukuza uchumi wa buluu. Walibainisha kuwa hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuongeza mapato kupitia uvuvi endelevu na matumizi ya zana za kisasa. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa sio tu kuinua kipato cha wavuvi wadogo lakini pia kuchangia kwa ukubwa kufikia malengo ya Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiwepo kuongeza uzalishaji wa samaki kutoka takriban tani 500,000 za sasa hadi tani 600,000 kufikia mwaka 2025/2025, kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa (GDP) kutoka asilimia 1.7 mpaka 1.9 ifikapo mwaka 2025/2026 na kuongeza ulaji wa samaki ambapo kwa sasa ni kilo 8.5 kwa mwaka kwa Mtanzania mmoja badala ya kilo 20 iliyowekwa Kimataifa.
Post a comment