WATAFITI KUTOKA TAFIRI NA DSFA WANASHIRIKI MAFUNZO YA MFUMO WA TATHMINI YA WINGI WA MAZAO YA UVUVI (WEIGHT OF EVIDENCE) MOMBASA, KENYA

Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) na Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), wanashiriki katika mafunzo ya mfumo wa tathmini ya wingi wa mazao ya uvuvi unaojulikana kama “Uzito wa Ushahidi” (Weight of Evidence), yanayofanyika Mombasa, Kenya. Mafunzo hayo yalianza tarehe 11 Novemba na yanatarajia kukamilizika Kesho tarehe 15 Novemba 2024.

Mafunzo haya yameandaliwa na Timu ya Tathmini na Usimamizi ya Idara ya Uvuvi na Ufugaji wa Viumbemaji ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na yanaendeshwa na Prof. Pedro Borros na Prof. Pedro Sousa. Lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya uvuvi katika kufanya tathmini ya hali ya uvuvi kwa kutumia njia shirikishi. Mbinu ya “Uzito wa Ushahidi” inayotumika kwenye mafunzo haya inajumuisha taarifa mbalimbali katika kufanya tathmini ya mazao ya uvuvi, kama vile takwimu za wingi wa samaki, ikolojia, Sayansi jamii na uchumi, na inalenga kutoa mwongozo wa vitendo kwa wataalamu kutoa ushauri bora wa usimamizi wa uvuvi. Mafunzo haya ni fursa muhimu kwa nchi zinazoendelea, hususan zile zenye changamoto za upungufu wa takwimu, uhaba wa fedha na wataalamu wa kutosha kufanya tathmini kwa kutumia njia anuwai.

Washiriki wa mafunzo haya wametoka Tanzania, Kenya, Namibia, Ushelisheli, Afrika Kusini, Madives, Msumbiji, Namibia, Ghana na Benin. Tanzania ina jivunia ushiriki wa watafiti watano kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ambao ni Dr. Catherine Mwakosya (Mtafiti Mwandamizi), Dr. Benedicto Kashindye (Kaimu Mkuu wa kituo cha TAFIRI Mwanza, Godfrey Rusizoka (Kaimu Meneja wa utafiti wa viumbe maji), Cecilia Mataba (Mtafiti), Said Mgeleka (Kaimu Meneja wa Utafiti wa Bahari), pamoja na Tumu Ali Mussa (Kaimu Meneja Usimamizi na Uhifadhi wa Uvuvi) kutoka Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DFSA). Ushiriki wa wataalamu hawa utaimarisha uwezo wa kitaifa wa kufanya tathmini za rasilimali za uvuvi na kuchangia katika maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi nchini. .

Post a comment