Tarehe 14 Desemba 2024, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imepokea ujumbe maalum kutoka Chiinese Academy of Science Geography and Limnology (NIGLAS) China ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Fedha na Usimamizi wa Mali Mr. LI Bin wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Sayansi Elimu na Utamaduni, Wizara ya Fedha Mr. LYU Jianping aliyevaa sweta jeusi kutoka upande wa kulia na Mkurugenzi wa Kituo cha Pamoja cha Utafiti cha Sino (SAROJEC) Profesa WANG Qingfeng wa pili mstari wa mbele kutoka kushoto aliyevaa T-shirt nyeupe. Ziara hii ililenga kutathmini mafanikio ya ushirikiano uliopo kati ya Taasisi hizi na kujadili maeneo mapya ya ushirikiano kwa maendeleo ya siku zijazo.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulipata fursa ya kuelezwa na kutembelea miradi mbalimbali ya utafiti inayotekelezwa na TAFIRI kwa kushirikiana na CAS na NIGLAS. Miongoni mwa mafanikio yaliyoangaziwa ni utafiti wa pamoja katika masuala ya ikolojia ya maji, uhifadhi wa viumbe maji, uchakataji wa sampuli za ikologia ya maji katika maabara za TAFIRI na teknolojia za kisasa za usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Akizungumza wakati wa kikao cha majumuisho, Naibu Mkurugenzi wa Fedha wa CAS alitoa pongezi kwa TAFIRI kwa juhudi zake za kiutafiti na mchango wake wa kitaaluma katika kushauri usimamizi wa rasilimali za maji na uvuvi nchini Tanzania. "Ushirikiano wetu umedhihirisha mafanikio makubwa, na tunatarajia kuyaimarisha zaidi kwa kuzingatia maeneo mapya ya utafiti na maendeleo," alisema. Kwa upande wa TAFIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei aliishukuru CAS na NIGLAS kwa mchango wao wa kifedha, kiutafiti na kujenga uwezo wa Taasisi kupitia mafunzo kwa watumishi na mbiundombinu Alisisitiza kuwa ushirikiano huu ni muhimu katika kuhakikisha dira ya TAFIRI ya kuwa Taasisi inayoongoza katika maswala ya utafiti wa uvuvi na viumbe maji Afrika. "Tunaamini kuwa kupitia ushirikiano huu, tutaweza kuongeza tija katika masuala ya utafiti na kuja na mbinu bora na za kisasa za uhifadhi wa mazingira ya majini, uvuvi endelevu na matumizi bora ya rasilimali za uvuvi," alisema. Katika kikao hicho, pande zote zilikubaliana kuchunguza maeneo mapya ya ushirikiano, ikiwemo utafiti wa mabadiliko ya tabianchi, teknolojia za kuhifadhi rasilimali za uvuvi, teknologia na maabara ya uchakataji wa sampuli na mbinu za kuongeza uzalishaji katika sekta ya uvuvi. Pia, zilikubaliana kuimarisha programu za mafunzo kwa watafiti na Maafisa Uvuvi wa TAFIRI kupitia fursa za mafunzo na ubadilishanaji wa wataalamu na uzoefu kati ya Tanzania na China .
Post a comment