Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imeandaa warsha ya siku moja kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake katika Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu katika Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi, iliyofanyika Jijini Dar es Salaam. Warsha hii ilifunguliwa na Dkt. Ismael Kimirei, Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, ambaye alisisitiza umuhimu wa watafiti kuwa wabunifu katika kutafuta mbinu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa ustawi wa Taifa .
Dkt. Kimirei alieleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri hifadhi za bahari na viumbe vilivyomo, na hivyo ni jukumu la wataalam kushirikiana katika kutafuta mbinu tunduizi zinazoweza kusaidia kupunguza athari hizi na kuhakikisha usimamizi bora wa mazingira ya bahari. Aliongeza kuwa mabadiliko haya yana athari kubwa za kiikolojia, na yanaweza kusababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa jamii na Taifa. Aidha, Dkt. Kimirei aliwahakikishia washiriki kuwa mradi wanaoutekeleza unashabihiana na juhudi za Serikali ya Tanzania zinazolenga kuwezesha wananchi kunufaika na Uchumi wa Buluu. DKt. Kimirei aliwaomba, wao kama jopo la wataalam kwenye eneo husika, wasisite kuzishauri serikali zao kuhusiana na matokeo ya utafiti wao. Pia, aliwafahamisha washiriki kuwa, TAFIRI kama mwenyeji wa mradi na Taasisi inayoshughulika na utafiti na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uvuvi endelevu, itahakikisha matokeo ya utafiti wao na mapendekezo watakayoyatoa yanafika kwenye vyombo vya maamuzi kwa wakati na kwa hatua stahiki. . Warsha hiyo ilijumuisha wataalam kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Ujerumani, na Australia, na ilihusisha mjadala kuhusu mbinu bora za kujumuisha taarifa za mabadiliko ya tabia nchi katika usimamizi wa hifadhi za bahari. Mradi wa Mustakabali wa Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Hifadhi za Bahari zilizopo Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi (CliMPA) ndio uliandaa warsha hii, huku lengo kuu likiwa ni kubuni mikakati ya kisasa ya kulinda bahari kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi. Mradi wa CliMPA ni wa miaka miwili na unafadhiliwa na Umoja wa Wanasayansi Bahari ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi (Western Indian Ocean Marine Science Association, WIOMSA). . Warsha hii iliwakutanisha wataalam wa hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi, ikolojia ya bahari, na usimamizi wa bahari kutoka taasisi za serikali na asasi za kiraia ili kujadiliana kuhusu changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazokabili hifadhi za bahari na jinsi ya kukabiliana nazo. Warsha hii ililenga kuhakikisha kwamba mipango ya uhifadhi wa bahari inazingatia mabadiliko ya tabia nchi na inabuni mbinu bora za kukabiliana na changamoto hizi kwa manufaa ya vizazi vijavyo. . Aidha, warsha ililenga kukuza ufahamu na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mazingira ya bahari; hivyo kuunga juhudi za nchi katika kulinda na kusimamia rasilimali za bahari ili zinufaishe Taifa na watu wake kupitia uchumi wa buluu. .
Post a comment