MH. DKT. SAMIA SULUHU AGAWA BOTI ZA KISASA NA VIZIMBA VYA KUFUGIA SAMAKI ZIWA VIKTORIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali imedhamiria kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Uvuvi, hivyo imeamua kutoa kipaumbele katika kukuza sekta hiyo kwa kuimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amebainisha hayo leo (30/01/2024) jijini Mwanza, wakati wa kukabidhi boti 160 na vizimba 222 kwa wanufaika kwenye Kanda ya Ziwa Victoria na kuitaka wizara kubuni mbinu zaidi za kuhakikisha inawezesha wanufaika wengi zaidi kupitia rasilimali za uvuvi.

Ameongeza kuwa kwa sasa wizara imekuwa ikifanya mambo mengi makubwa na yenye kuleta tija kwa wananchi ambapo katika Sekta ya Uvuvi wananchi wengi wamekuwa wakitegemea sekta hiyo kwa ajili ya kujipatia kipato.

Amewataka pia walionufaika wa boti za uvuvi na vizimba kuhakikisha wanatumia vyema zana hizo na kuzitunza pamoja na kuondokana na migogoro yoyote ambayo inaweza kujitokeza kwenye vikundi vyao kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha mradi huo unaenda maeneo mengi zaidi hapa nchini.

Aidha, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024 wizara hiyo ilipatiwa fedha Shilingi Bilioni 60 kila mwaka kwa miaka miwili mfululizo katika kukuza Sekta ya Uvuvi.

Pia Mhe. Ulega amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 nia ya wizara ni kusambaza boti za uvuvi zisizopungua 500 kote nchini ili kuwezesha wanufaika wengi zaidi kwa kuwa Sekta ya Uvuvi inatoa ajira kwa zaidi ya watu Milioni 4.5.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bw. Frank Nyabundege amesema Mwaka 2022 Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssan aliipatia benki hiyo Shilingi Bilioni 210 ambapo nia ya Mhe. Rais ni kuhakikisha benki hiyo inakua na kutatua changamoto mbalimbali kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Amesema kupitia boti 55 zilizokabidhiwa kwa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya shughuli za uvuvi zitanufaisha vijana zaidi ya 1,500 na kwamba mikopo ya boti na vizimba inatolewa bila riba hivyo TADB inatarajia kadri mikopo hiyo itakayovyokuwa inarudishwa itawanufaisha wengi zaidi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema wizara itahakikisha inaendeleza maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inazidi kutoa ajira zaidi kupitia zana mbalimbali zikiwemo boti na vizimba ambavyo amevigawa leo kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji kupitia mkopo usio na riba.

Prof. Shemdoe ameongeza kuwa kupitia boti na vizimba vijana watapata fursa ya kujipatia ajira pamoja na kuongezea vipato kupitia ufugaji wa samaki na kwamba kupitia mradi huo jitihada mbalimbali zitaendelea kufanywa ili kufikia wanufaika wengi zaidi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makala amesema hafla ya kukabidihi boti 55 na vizimba 222 kwa mkoa huo, utakuza uvuvi endelevu kwa kuwa amekutana na wadau wa uvuvi ambapo tafiti zinaonesha samaki ndani ya Ziwa Victoria wamepungua kwa asilimia 30 na kuathiri baadhi ya viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, kutokana na kukithiri kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu na kwamba mkoa tayari umeweka mikakati mbalimbali kudhibiti vitendo hivyo.

Mhe. Makala ameongeza kuwa kitendo cha kuwakabidhi wavuvi boti kitasaidia kukuza uvuvi endelevu na kwamba elimu imekuwa ikiendelea kutolewa kwa wakazi wa mkoa huo kufuga samaki kwa njia ya vizimba ili kukuza soko la samaki.

Nao baadhi ya wanufaika wa boti na vizimba wameshukuru kwa kupatiwa zana hizo pamoja na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki, wameiomba serikali kuwahakikishia mbegu bora za vifaranga vya samaki pamoja na chakula ili waweze kufuga kibiashara na kukuza kipato chao na hatimaye kuweza kurejesha mikopo.

Pia wamesema wamefurahia kupatiwa boti za kisasa na zenye injini za kupachika ambazo ni imara hivyo watahakikisha wanatumia vyema boti hizo ili waweze kurejesha mikopo na kuweza kukopa kwa awamu nyingine.

Post a comment