VIONGOZI KUTOKA IDARA YA UVUVI, WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI WATEMBELEA BANDA LA TAFIRI KATIKA MAONESHO YA NANENANE 2024 DODOMA

Leo Tarehe 05 Agosti, 2024: Viongozi kutoka Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Baraka Sekadende (Wa pili kulia) na Bw. Chris Nzowa (Wa pili kushoto), wametembelea Banda la Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ili kujionea shughuli za Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo NaneNane 2024, yanayoendelea katika viwanja vya Maonesho,Nzuguni, Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Dkt. Sekadende na Bw. Nzoa walipata fursa ya kujionea na kupata maelezo kuhusu teknolojia na mbinu mpya za utafiti wa uvuvi zinazotumika TAFIRI, pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia tafiti hizo. Maonesho ya NaneNane mwaka huu yana kauli mbiu inayosisitiza umuhimu kuchagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo, na uvuvi.

Kwa upande wake, Dkt. Sekadende alieleza kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyofikiwa na TAFIRI katika sekta ya uvuvi na kupongeza juhudi za watafiti katika kuboresha uchumi wa nchi kupitia kilimo na uvuvi. Bw. Nzoa aliongeza kuwa ziara hiyo imempa mwanga na hamasa zaidi katika kuendeleza sekta ya uvuvi hasa kupitia ushirikiano na taasisi kama TAFIRI.

Maonesho ya NaneNane 2024 yamejumuisha washiriki kutoka sekta mbalimbali za kilimo na uvuvi, wakiwemo watafiti, wakulima, na wadau wa sekta hizi muhimu kwa uchumi wa Tanzania.

Post a comment